Zaidi
ya watu 250 wanapata ulemavu wa kudumu kila mwaka nchini kutokana na
kuugua ugonjwa wa ukoma hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na
waathirika kutengwa na kunyanyapaliwa na jamii licha ya maradhi hayo
kutibika endapo mtu atakayegundulika kuwa nayo atawahi kupata matibabu
mapema.
Hayo yamebainishwa na waziri wa afya maendeleo ya jamii jinsia
watoto na wazee Ummy Mwalimu wakati akitoa tamko la wizara kuhusu
maadhimisho ya siku ya ukoma duniani ambapo amesema kwa mujibu wa
takwimu zilizotolewa mwaka 2014 jumla ya watu 2134 nchini waligundulika
kuwa na maradhi hayo huku 271 kati yao ambao ni sawa na asilimia 13
wakipata ulemavu wa kudumu kutokana na kukatika kwa baadhi ya viungo
vyao.
Beatrice Mutayoba ni meneja wa mpango wa kudhibiti kifua kikuu na
ukoma kutoka wizarani ambapo anasema ugonjwa wa ukoma bado upo kwenye
halmashauri 17 nchini mbili kati ya hizo zikiwa Tanzania Zanzibar huku
mikoa ya Lindi na Mtwara ikiongoza na historia inaonyesha tangu
kugundulika kwa maradhi ni maeneo hayo tu ndio yamekuwa yakiripotiwa
kuwepo kwa maambukizi ya juu bila kuwepo kwa sababu za kitaalamu.
Kwa upande wake Dk Deus Kamara mratibu wa kudhibiti ukoma na kifua
kikuu akizungumzia kuwepo kwa makambi ya wagonjwa wa ukoma ambayo
yanadaiwa kutelekezwa na serikali amesema tayari makambi hayo
yalishafungwa zaidi ya miaka 10 iliyopita lakini watu waliokuwa wakiishi
kwenye makambi hayo wameendelea kuishi kutokana na jamii kuwatenga
hivyo hawana mahala pa kwenda.
Tanzania ni miongoni mwa nchi 17 duniani ambazo bado zina
maambukizi ya ugonjwa wa ukoma ambao waathirika wake wanashindwa
kushiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo za kiuchumi na kusababisha
hasara kwa familia na taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment