1. Utangulizi
Kumekuwepo
na taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya Kitaifa na
Kimataifa kuhusu Homa ya Zika ambao ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi
kijulikanacho kama “Zika Virus”.
Ugonjwa
huu uligundulika kwa mara ya kwanza nchini Uganda katika miaka ya 1947
kwenye wanyama aina ya sokwe/nyani (rhesus macaque) ndani ya Misitu ya
Zika, karibu na Ziwa Victoria.
Mnamo
mwaka 1952, ugonjwa wa zika uligundulika kwa binadamu nchini Uganda na
Tanzania, na mwaka 1968 uligunduliwa nchini Nigeria.
Kuanzia
mwaka 1951 hadi 1981, ugonjwa huu umeshatolewa taarifa katika nchi
takribani sita (6) za Afrika ambazo ni Afrika ya Kati, Egypt, Gabon,
Sierra Leone, Tanzania na Uganda.
Vile
vile, ugonjwa huu umeshatolewa taarifa katika nchi za India, Indonesia,
Malaysia, Philipine, Thailand na Vietnam na pia nchi za Amerika na
Pacific.
Kuanzia
mwezi Mei 2015, ugonjwa huu ulianza kutolewa taarifa ambapo hadi sasa
umeathiri zaidi Bara la Amerika ya Kusini. Kuna takribani nchi 22 ambapo
Wagonjwa wamethibitishwa kimaabara kuwa na ugonjwa wa Zika. Nchi hizo
ni Brazil (Majimbo 14 yameathirika), Colombia, Suriname, El Salvador,
Guatemala, Paraguay, Mexico, Venezuela, Panama, Cape Verde, Honduras,
Panama, France (French Guiana na Martinique, United States of America
(Puerto Rico), Guyana, Barbados, Ecuador, Bolivia, Haiti, Ujerumani,
France (Saint Martin and Guadeloupe na Dominican Republic.
Ugonjwa
huu unaenezwa na mbu aina ya Aedes ambaye (huwa ana tabia ya kuuma
asubuhi na pia nyakati za mchana/jioni). Aina hii ya kirusi ipo katika
familia ya “Flavirus” ambapo pia wapo virusi vya ugonjwa wa Dengue, Homa
ya Manjano (Yellow Fever), Japanese ancephalitis na West Nile Virus.
Kirusi
cha homa ya Zika kama kile cha Dengue kinaambukizwa kutoka mtu mmoja
hadi mwingine kwa kuumwa na mbu wa jamii ya Aedes hasa Aedes aegypti.
Mbu huyu anaishi katika mazingira ya makazi ya binadamu, huuma wakati wa
mchana ndani ya nyumba au kwenye maeneo yenye viwili, hususani majira
ya asubuhi na jioni kabla ya jua halijazama.
Mbu
huyu anazaliana katika maji yaliyotuama hasa kwenye vyombo vya
nyumbani, makinga maji ya paa za nyumba, matairi ya gari, ndoo, makopo
nk.
2. Dalili za Homa ya Zika
Dalili
za ugonjwa huu zinafanana na za homa ya Dengue, ambazo ni homa, kuumwa
na kichwa, maumivu ya viungo, macho kuwa mekundu na vile vile kupata
vipele vidogo vidogo kama harara (Skin rashes).
Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati siku ya 2 hadi 7 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya Zika.
Uko
uwezekano, ambao haujathibitishwa rasmi, kwamba wakati mwingine
wagonjwa wanaweza kupata matatizo katika ubongo (Neurological
Complications) na miguu kupooza (Gullein Barre Syndrome), na wajawazito
huweza kujifungua watoto wenye ulemavu wa kichwa yaani kichwa kuwa
kidogo kulingana na umri wa mtoto (microcephaly).
Kwa
wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili
za malaria. Hivyo basi, natoa rai kwa wananchi kuwa, wakati
wanapojisikia homa au wamepata homa wahakikishe wanapima ili kugundua
kama wana vimelea vya malaria au la, kwa kuwa dalili za ugonjwa wa Zika
zinaweza kufanana sana na dalili za malaria.
Homa
ya Zika inaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na
kupatiwa matibabu ya haraka. Hakuna dawa maalum ya ugonjwa huu wala
chanjo bali mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na
ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji na damu.
Mara
tu baada ya kuwepo kwa taarifa juu ya ugonjwa huu, Serikali kupitia
Wizara ya Afya imefanya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika vituo vya
kutolea huduma za afya nchini pamoja na mipakani kupitia mfumo wa
ufuatiliaji wa magonjwa (surveillance system ya Wizara).
Tumejiridhisha
kuwa ugonjwa wa homa ya Zika kwa sasa haujaingia nchini kwetu. Hivyo,
Wananchi wasiwe na hofu ila waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya
ugonjwa huu pamoja na magonjwa ya Dengue na Malaria kwa ujumla ikiwa ni
pamoja na kuzingatia yafuatayo:-
(i) Kuangamiza mazalio ya mbu kwa:
kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au kunyunyizia viuatilifu vya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo.
kuondoa
vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile; vifuu vya nazi,
makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo, nk.
kufyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu.
Kuhakikisha kuwa maua yanayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama.
Kufunika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara.
kusafisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama.
(ii) Kujikinga na kuumwa na mbu kwa;-
Kutumia viuatilifu vya kufukuza mbu “mosquito repellants”
Kuvaa nguo ndefu ili kujikinga na kuumwa na mbu.
Kutumia vyandarua vilivyosindikwa viuatilifu (kwa wale wanaolala majira ya mchana hasa watoto).
kuweka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi.
4. Hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara ni pamoja na:-
1.Tanzania
ikiwa ni nchi mwanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) inaendelea
kuwasiliana na kushirikiana kwa karibu na Shirika la afya Duniani –
Ofisi ya Tanzania kwa lengo la kupata Taarifa na maelezo zaidi ya
kukabiliana na ugonjwa huu. Kamati ya Dharura ya Miongozo ya Kimataifa
ya Afya ya WHO yaani “International Health Regulations Emergency
Committee” itakutana siku ya Jumatatu ya tarehe 1/2/2016, mjini
Geneva,Uswisi ili kufanya tathmini ya ugonjwa huo na kutoa tamko na
maelekezo zaidi ya namna ya kudhibiti Ugonjwa huu kwa nchi wanachama.
Baada
ya tamko/Mwongozo huo wa WHO, Wizara ya Afya itaandaa Taarifa ya
tahadhari ya ugonjwa huu kwa ajili ya kusambazwa kwa Waganga Wakuu wote
wa Mikoa na Wilaya Tanzania Bara. Aidha, taarifa hii itajumuisha namna
mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (ainisho la Ugonjwa), “Ukweli Kuhusu
Ugonjwa” (Fact Sheet), Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya
kuchukua sampuli. Vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga na
maambukizi ya ugonjwa huu vitatolewa.
2.
Wizara itaanza kutoa elimu kwa wananchi kupitia Radio na Runinga kuhusu
ugonjwa huu sambamba pia na ugonjwa wa Dengue ambao uambukizi wake
unasababishwa na Mbu aina ya Aedes.
3. Kuendelea kutoa vyandarua vyenye uatilifu katika Mkoa yote Tanzania ili kufikia lengo la asilimia 95.
4.
Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika vituo vya kutolea huduma
za afya pamoja na mipakani kupitia mfumo wa surveillance ya Wizara.
Aidha, Wizara inatoa maelekezo kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya hapa
nchini kutoa taarifa za watoto watakaozaliwa wakiwa na ulemavu wowote
wa kichwa ikiwemo “microcephaly” au “anencephaly”.
5.Kufuatilia
kwa karibu ongezeko la wagonjwa wenye homa isiyokuwa ya malaria kwa
Mikoa na Wilaya zote nchini ili kuweza kufanya uchunguzi wa kina iwapo
kuna ugonjwa huu.
6.
Kuimarisha uwezo wa kutambua ugonjwa huu kwa kina kupitia maabara ya
Taifa iliyopo katika Taasisi ya uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu
(NIMR). Wizara itashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Shirika la
Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (Centre for Disease
Control (CDC) katika kuhakikisha kuwa vitendanishi vya kutambua ugonjwa
huu vinapatikana.
7.
Kushirikisha program ya Malaria na NIMR katika kudhibiti mbu kwa
kupulizia na kunyunyizia viuatilifu. Hii inalenga kuangamiza mbu
wapevu na viluwiluwi.
5. Hitimisho
Ugonjwa
wa Homa ya Zika bado haujaingia Tanzania. Wananchi waondoe hofu juu ya
uwepo wa ugonjwa huu. Hata hivyo, ni muhimu kwa kila mmoja wetu
kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya Zika, Dengue na
malaria ambayo huenezwa kwa namna inayofanana.
Aidha,
mvua hizi kubwa zinazoendelea kunyesha hapa nchini zinaweza kuchangia
kuongezeka kwa mazalio ya mbu. Hivyo, utupaji, uzoaji na uhifadhi wa
taka katika vijiji na miji yetu ni lazima uimarishwe katika kuhakikisha
mazingira yetu yanakuwa salama kwani bila ya kuzingatia hayo, tunatoa
fursa kwa mazalio ya mbu kuongezeka na hata kuwa karibu zaidi ya makazi
ya binadamu.
Wizara
ya Afya itaendelea kutoa taarifa za mara kwa mara kwa wananchi ili
waweze kuelewa kuhusu ugonjwa huu na kuchukua hatua stahiki.
Imetolewa na:-
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
31/1/2016
No comments:
Post a Comment